MAFUNDISHO YA MWAKASEGE
HONGERA KWA KUOKOKA
HONGERA KWA KUOKOKA
UTANGULIZI
Karibu kwenye Ufalme wa Mungu
Kitabu hiki kimeandikwa kwa ajili yako. Roho Mtakatikfu amekiweka mikononi mwako kwa kusudi muhimu la Mungu ndani ya Kristo.
Katika Jina lile lipitalo majina yote jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu, napenda kukukaribisha katika Ufalme wa Mungu!
Imeandikwa wazi kabisa katika kitabu cha Waefeso 2:19 ya kuwa; “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”.
Umepata neema hii ya Mungu, na sasa umeokoka – biblia inakuambia tangu sasa wewe si mgeni wala mpitaji katika Ufalme wa Mungu - bali wewe ni mwenyeji pamoja na watakatifu wengi waliomo katika nyumba ya Mungu!
Nia ya Roho Mtakatifu kukuwekea kitabu hiki mikononi mwako, ni kukufahamisha angalau kwa kiasi fulani juu ya uamuzi uliofanya wa kutubu dhambi zako, na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako.
Kitabu hiki kitakusaidia kujua kitu gani kimetokea ulipookoka na mambo muhimu ya kufanya katika maisha hayo mapya ya wokovu.
Umefanya uamuzi wa busara – katika Luka 15:10 biblia inatuambia ya kuwa hata malaika wa mbinguni wanashangilia na kuufurahia uamuzi huo uliofanya.
Na mimi kama mtumishi wa Mungu aliye hai napenda kumshukuru Mungu katika Kristo Yesu kwa kukufunulia siri hii ya wokovu ambayo wengi hawajaiona na wengine wameiona lakini wanaipuzia. Ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa atakutia nguvu na kukupa ufahamu wa rohoni unapokisoma kitabu hiki ili kikusaidie katika maisha yako ya kila siku.
Christopher na Diana Mwakasege ,
S.L.P. 2166,
ARUSHA
UMEFANYA UAMUZI WA BUSARA
Umefanya uamuzi wa busara. Ndiyo! – tena ni kweli kabisa. Umefanya uamuzi wa busara. Umeamua kutubu dhambi zako kwa Mungu, na kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama Bwana na Mwokozi wako – umefanya uamuzi wa busara. Naamini pia ya kuwa uamuzi huu uliofanya ni uamuzi wa kudumu.
Nimeona nikutie moyo namna hii kwa kuwa mtu anapookoka wakati mwingine anasumbuka na mawazo na kujiuliza maswali mengi – akijiuliza ikiwa kwa kuokoka amefanya uamuzi sahihi. Watu wengine kwa kutopata majibu sahihi ya swali hili wanakata tamaa na kurudi nyuma kiroho – na hata wapo wengine wanaoamua kuacha wokovu kabisa.
Nakutakia heri kwa Bwana na kumwomba Mungu azidi kujifunua wazi zaidi kwako ili usiwe kati ya wale wanaokata tamaa na kuacha wokovu. Umeifanya sala ya toba kwa moyo wako wote na umeokoka – ni uamuzi wa busara mtu yeyote asikudanganye wala kukukatisha tamaa.
Umechagua Baraka!
Umechagua kuokoka kwa kumwamini na kumpokea Yesu Kristo kama mwokozi wako,maana yake umechagua baraka.
Inawezekana hukujua lakini mtu ambaye hajaokoka anaishi chini ya laana, na mara anapookoka – Yesu Kristo anamtoa kwenye laana nakumwingiza ndani yake – ambaye ndiye Baraka na chanzo cha baraka zote za Mungu.
Tangu zamani Mungu alimpa mtu uhuru wa kuchagua kati ya baraka na laana aliposema
“ Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana Mungu wenu…. Na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya Bwana…. (Kumbukumbu la Torati 11:26-28)
Umechagua kuokoka – umechagua baraka! Baraka maana yake, furaha, amani, kufanikiwa, kustawi, kukua,kunawiri na kunona!
Ndiyo maana Mtume Paulo aliandika katika kitabu cha Waefeso 1:3 hivi, “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.”
Huu mstari unazungumza juu yako pia kwa kuwa unapookoka unaingia “ndani yake Kristo”. Kwa kuwa ulipookoka uliingia ndani yake Kristo, kwa hiyo umebarikiwa kwa baraka zote za rohoni!
Unaweza ukajiuliza kama ni baraka zote za rohoni je za kimwili na za akili nitazipataje? Fahamu neno hili baraka zote zimeanza rohoni!
Ndiyo maana imeandikwa hivi katika kitabu cha Wagalatia 3:13, 14 kuwa; “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu, maana imeandikwa amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti, ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya roho kwa njia ya amani”.
Ndani ya baraka ya Ibrahimu tunayoipata katika Kristo Yesu kuna mafanikio katika maisha ya sasa na ya baadaye – baada ya kufa. Ukiokoka unaanza kubarikiwa ukiwa hapahapa duniani!
Hakuna hasara!
Umefanya uamuzi wa busara ulipoamua kuokoka kwa sababu ndani ya Yesu Kristo hakuna hasara. Wewe uwe mtendaji wa neno lake, na ndipo utakapojua na kuthibitisha ya kuwa kweli kwa Yesu Kristo kuna kila kitu unachokihitaji sasa na cha maisha ya siku zote.
Inawezekana umewahi kusikia watu wakisema mtu anapookoka anafilisika – na inawezekana umewahi kuona watu wengine waliookoka wakiwa na maisha duni. Nataka nikueleze ya kwamba haimo katika mpango wa Mungu kuwafilisi watu wake wanapookoka. Wengi wanakuwa na maisha duni kwa sababu ya kukosa mafundisho sahihi ya neno la Mungu baada ya kuokoka! Wanaangamia kwa kukosa maarifa ya neno la Mungu.
Ukichukua biblia yako na kusoma kitabu cha 2Wakorintho 8:9 utaona wazi wazi ya kuwa kati ya mambo aliyoyafanya Yesu msalabani alipokufa kwa ajili yetu – ni kuuchukua umaskini wetu ili tupate kupokea utajiri wake.
Ndiyo sababu Yesu Kristo aliwahi kuwaambia wanafunzi wake (ambao ni pamoja na wewe sasa kwa kuwa umeokoka) ya kwamba:
“ Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:29,30).
Haya ni maneno ya Yesu Kristo mwenyewe, na Roho Mtakatifu anakuletea maneno haya ndani ya moyo wako kukuondoa wasiwasi. Umeamua kuokoka – umeamua kupokea baraka kuanzia sasa.
Nataka nizidi kukutia moyo ya kuwa umefanya uamuzi wa busara kwa kuokoka. Maana umechagua baraka umeikataa laana; umechagua Uzima, umeikataa mauti; Umechagua Nuru, Umeikataa giza; Umemchagua Yesu, umemkataa shetani;Umechagua kwenda mbinguni, umekataa kwenda jehanamu!
Hata kufahamu ya kuwa ulipookoka umefanya uamuzi wa busara – ni baraka ya pekee pia! Au wewe unasemaje? – ni kweli au uongo?
Kumbuka unapookoka unampokea Yesu Kristo moyoni mwako ambaye ndiye KWELI kwa hiyo nakushauri kataa uongo unaotaka kukurudisha nyuma kiroho. Umeamua kuokoka – umeamua kwa busara na uwe ni uamuzi wa kudumu!
KITU GANI KIMETOKEA ULIPOOKOKA?
Mtume Paulo alipokuwa anawaandikia Wakorintho katika waraka wa kwanza sura ya kumi na tano na mstari wa tatu, juu ya kufa na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo alisema;
“Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe; ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na yakuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko”.
“Kama yanenavyo maandiko” – ni maneno ambayo Mtume Paulo ameyatumia mara mbili katika mstari huu wa biblia, - akiwa na nia ya kuwaonyesha wasomaji kuwa chanzo cha maelezo yake juu ya kufa, na kuzikwa na kufufuka kwa Kristo ameyasema sawa na MAANDIKO.
Ukitaka kujua kitu gani kimetokea ulipoamua kuokoka, ni muhimu tusome maandiko – bibilia kuona inasemaje juu ya hali yako sasa.
Katika sura hii ya tatu ya kitabu hiki nataka nikupe baadhi ya maandiko katika biblia ambayo yatakusaidia kujua kilichotokea ulipookoka:
1. Umesamehewa dhambi zako zote!
“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu…. Aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani …” (Wakolosai 2:13,14).
“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9).
2. Jina lako limeandikwa mbinguni!
“…furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni” (Luka 10:20).
“Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake” (Ufunuo 3:5).
3. Umekuwa kiumbe kipya!
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).
“Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiri, bali kiumbe kipya” (Wagalatia 6:14,15).
“Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu, mkavae utu mpya ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli” (Waefeso 4:22-24).
4. Umekuwa mtoto wa Mungu!
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu (Yohana 1:12,13).
“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo… Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yohana 1:1,2).
5. Malaika wamekuzunguka hata kama huwaoni!
“Je! hao wote (malaika) si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaorithi wokovu? (Waebrania 1:14).
“Kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (Zaburi 91:11,12)
6. Umekuwa makao ya Kristo na Mungu!
“Yesu akajibu, akamwambia, mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23)
“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu” (Wagalatia 2:20).
“Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Waefeso 2:22).
7. Roho Mtakatifu yumo ndani yako sasa!
“Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).
“Au hamjui ya kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? (1Wakorintho 6:19).
8. Una mamlaka juu ya shetani na kazi zake tangu sasa!
“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru” (Luka 10:19)
“Na ishara hii zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo …. Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:17,18).
“Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).
9. Utafufuliwa au kunyakuliwa Yesu akija kulichukua kanisa maana unao uzima wa milele!
“Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima” (1Yohana 5:12).
“Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1Wathesalonike 4:16,17).
“Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu …. (Ufunuo 20:6
Haya ni baadhi tu ya maneno mengi mazuri ambayo yamo katika biblia yanayoeleza kilichotokea ulipookoka. Nakupa ushauri ya kuwa uyasome mara kwa mara pamoja na mengine yaliyomo katika biblia ili upate kujijua wewe sasa ni nani mbele za Mungu na za shetani baada ya kuokoka.
USIOGOPE KUSEMA JUU YA UAMUZI WAKO
“Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike…. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu” (1Petro 3:14-15)
Je! unaogopa kuwaambia ndugu zako, majirani zako au rafiki zako ya kuwa sasa umeokoka, na Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako?
Je! unaogopa kuwaeleza watu waziwazi ukiulizwa juu ya mabadiliko ya tabia yako ya kuwa sasa wewe ni “kiumbe kipya”?
Je! unababaika na kushindwa kujibu ukiulizwa ikiwa umeokoka? Maana inawezekana hata wewe ingawa umeokoka kweli, lakini ukiulizwa kama umeokoka unababaika na kusita kusema uhusiano wako mpya na Yesu Kristo.
Kuna wengine hata wanadiriki kuishi maisha ya kinyonga. Akiwa katikati ya kundi la watu waliookoka, kwake inakuwa rahisi kusema ya kuwa ameokoka. Na akiwa katikati ya kundi la watu wasiokoka, anashindwa kuonyesha msimamo wake hata kama akitakiwa kufanya hivyo.
Je! unayafahamu madhara ya maisha ya namna hii? – yapo madhara yake kwako. Ndiyo maana biblia inasema.” Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike… mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.”
Kuna madhara yake ukiogopa kumkiri Yesu mbele ya watu ya kuwa ni mwokozi wako – yapo madhara.
Yesu Kristo mwenyewe alisema hivi juu ya jambo hili, maana alijua litatokea jambo kama hili;
“Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 10:32,33).
Yesu Kristo hapa anazungumza juu ya maisha ya sasa. Kumbuka Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba, na huko anatuombea na ndiye mtetezi wetu.
Hakuna namna ambavyo utasikilizwa maombi yako na Baba Mungu na kupata msaada unaouhitaji bila msaada wa Yesu Kristo. Kwa hiyo mojawapo ya madhara ya kumkana Yesu mbele za watu ni kwamba na wewe ukihitaji akutaje mbele za Baba ili ujibiwe maombi yako na yeye atakaa kimya.
Ingawa ni kweli unapookoka, Mungu anakutumia malaika wa kukuhudumia na kukulinda, lakini ukiona aibu kumkiri Yesu mbele za watu unapotakiwa kuonyesha msimamo wako kiroho – malaika nao hawakusaidii – kwa sababu malaika wanakusaidia kwa sababu ya neno la Kristo juu yako kwao. Yesu akikaa kimya, na malaika wanakaa kimya! Ndiyo maana Yesu Kristo alisema;
“Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu” (Luka 12:8,9).
Fikiria upo katikati ya majaribu, na unahitaji msaada wa Mungu; halafu malaika wanaokuzunguka wanamuuliza Yesu Kristo kama wakusaidie au la – Yesu Kristo atakaa kimya asiseme kitu au anaweza kukukana mbele ya hao malaika ikiwa utakuwa na tabia ya kumwonea aibu na kumkana mbele za watu.
Na majaribu yatakusonga na kukuangusha, utadhani ya kuwa Mungu hasikii maombi yako. Lakini ni vizuri ufahamu utaratibu huu wa kusaidiwa na Mungu ya kuwa ukiogopa kumkiri Yesu Kristo mbele ya watu (ndugu zako au rafiki zako) ya kuwa ni Bwana na Mwokozi wako, siku ukihitaji msaada wa Mungu Yesu atakaa kimya, Baba Mungu atakaa kimya na malaika watakaa kimya.
Ukitaka msaada wa haraka katika majaribu hasa ya kuanguka dhambini usione haya kumkiri Yesu mbele za watu ya kuwa ni Bwana na Mwokozi wako. Mungu atakupa haraka njia na hekima ya kutoka katika hayo majaribu.
Nimeona watu wengi waliookoka wakirudi kuvuta sigara kwa sababu hawakuwaeleza rafiki zao ya kuwa wameokoka, walipokaribishwa kuvuta sigara walishindwa kukataa na walishindwa kuwaambia rafiki zao ya kuwa Yesu ni Mwokozi wao kwa hiyo hawavuti sigara tena.
Vivyo hivyo nimeona watu wengine waliookoka wakirudi kunywa pombe kwa sababu waliona aibu kuwaeleza ndugu zao na rafiki zao ya kuwa wameokoka na Yesu ni Bwana na Mwokozi wao, kwa hiyo hawatakunywa pombe tena. Lakini kwa kuona aibu kumkiri Yesu mbele ya watu wanaowakaribisha pombe – wanaanguka kwenye ulevi tena.
Nimeona pia watu wengi waliookoka – hasa wasichana na wanawake wakianguka katika uasherati kwa sababu ya kutowaambia wanaume wanaowasumbua ya kuwa wameokoka na hawataki utani wala kuharibu maisha yao ya kiroho kwa uzinzi. Wengi wa wale nilioweza kuzungumza nao kama wangekuwa wamefuata misingi ya neno la Mungu ya kutomwonea haya mwana wa Adamu – wasingeanguka katika zinaa.
Tatizo lilipo
Kinachowafanya wengi waogope kumkiri Yesu Kristo mbele za watu ni kwa sababu wanaogopa kuchekwa au kuzomewa au kutengwa na jamii au rafiki au ndugu; wengine wanaogopa kupigwa na wazazi wao au waume zao; wengine wanaogopa kufukuzwa kazi; na kadhalika, ili mradi kila mtu anayo sababu ya kujitetea kwa nini anashindwa kusema ameokoka.
Lakini hawajui baada ya muda wanapoa kiroho na kurudi nyuma kabisa; hata wengine kuacha wokovu kwa sababu hawana msaada wowote wa kuyashinda majaribu.
Biblia inasemaje juu ya jambo hili? Biblia imezungumza mengi juu ya jambo hili na baadhi ya mistari hiyo ni hii:
“Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike…. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu” (Petro 3:14,15)
Yesu Kristo alisema hivi;
“Heri wenye kuudhiwa kwa sababu ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mathayo 5:10-12)
Unaweza kuikosa mbingu
Usifanye mzaha kwenye wokovu. Uamuzi ulioufanya wa kuokoka ni uamuzi wa busara – lakini pia ni uamuzi wa ‘kufa na kupona’. Maana shetani amekukasirikia lakini usiogope kwa sababu yeye aliye ndani yako ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia (1Yohana 4:4)
Kwa kuwa umeamua kuokoka bila kulazimishwa, basi usione aibu kumkiri Yesu Kristo mbele za watu ya kuwa ni Bwana na Mwokozi wako.
Kwa sababu ukimwonea aibu sasa, siku atakapokuja kuchukua wateule wake – wewe utaachwa! Hutanyakuliwa! Ndivyo Yesu Kristo mwenyewe alivyosema:
“Akawaambia wote, mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate ….kwa sababu kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, na atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu” (Luka 9:23,26).
Kwa nini ukubali kuupoteza ufalme wa mbinguni kwa kuwaogopa wanadamu? Ndiyo maana Mtume Petro aliongozwa na Roho wa Mungu kutuandikia maneno haya ya kututia moyo aliposema; “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoshiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.
“Mkilaumiwa kwa ajili ya Jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa Utukufu na wa Mungu anawakalia. Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine. Lakini ikiwa kwa sababu ni mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo” (1Petro 4:12-16)
Kumbuka ya kuwa hata kama ndugu zako au rafiki zako au wanaokuzunguka hawafurahii kuokoka kwako – mbinguni wanafurahi – malaika pia wanafurahia – soma mwenyewe katika kitabu cha Luka 15:7,10.
Kama ulikuwa na aibu ya kumkiri Yesu mbele za watu, nakushauri sasa hivi utubu na Mungu atakusamehe, halafu mwombe Mungu akupe ujasiri na hekima ya namna ya kumkiri mbele za watu bila kuona haya kila nafasi inapotokea.
Sema hivi unaposali (ikiwa unapata shida juu ya namna ya kutubu).
“Mungu Baba nisamehe kwa kumwonea haya mbele za watu Mwana wako Yesu Kristo aliye Mwokozi wangu. Nitakase kwa upya kwa Damu yake na Neno lake. Naomba unipe ujasiri na hekima ili nijue kumjibu kila mtu juu ya wokovu ulionipa. Kwa jina la Yesu Kristo nimeomba na kuamini ya kuwa umenisikia – Amina”.
UHAKIKA WA WOKOVU WAKO
Ni rahisi sana kufika wakati mwingine ukajihukumu mwenyewe, na hata kufikiri labda hujaokoka sawasawa.
Pia, unaweza ukahukumiwa na watu wengine wakikuambia hujaokoka sawasawa wakitoa sababu nyingi wanazojua wao – na usipokuwa na maandiko ya kutosha unaweza kubabaika sana – na msimamo wako wa kiroho kuyumba.
Utapataje uhakika wa wokovu wako? Utajuaje ya kuwa kweli umeokoka – hata wakati wengine wanakwambia hujaokoka sawasawa – tena wengine wameokoka siku nyingi kabla yako?
Yesu Kristo alisema; “ Tena mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32). Alikuwa ana maana gani alipokuwa anasema tutaifahamu kweli? ‘Kweli’ maana yake nini? Yesu alipokuwa akifanya sala katika Yohana 17:17 alisema; “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli”.
Naamini kweli utakayoifahamu katika sura hii, itakuweka huru – tena utakuwa huru kweli kweli!
Mambo mawili makubwa yafuatayo yatakusaidia kupata uhakika wa wokovu wako;
1. Kujua ya kuwa umesamehewa dhambi zako na Mungu hazikumbuki tena;
2. Kujua ya kuwa Roho Mtakatifu aliye ndani yako ni muhuri wa Mungu wa kuonyesha ya kuwa wewe tayari ni wake milele!
Sasa na tuangalie kwa kifupi jambo moja moja.
1. Juu ya Msamaha wa dhambi
Unahitaji kujua na kuwa na uhakika siku ile uliyotubu kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako, dhambi zako ZILISAMEHEWA, ZILIFUTWA, WALA MUNGU HAZIKUMBUKI TENA.
Ndiyo Mungu hazikumbuki tena! Ndivyo neno lake linavyosema. Hebu tafakari mistari ifuatayo:
“Haya, njooni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu” (Isaya 1:18).
Tena Mungu alisema hivi katika Isaya 43:25;
“Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako”.
Mungu anasema hatazikumbuka tena dhambi zako! Sasa wewe kwa nini dhambi ulizokwisha kuzitubu bado zinakusumbua rohoni? – Inakuwa kama vile Mungu hajakusamehe!
Lakini nakwambia ya kuwa ikiwa ulitubu katika roho na kweli – umesamehewa dhambi zako – wala Mungu hazikumbuki tena! Kwa hiyo na wewe usizikumbuke tena! Hata kama mawazo yako yanakuzomea – hata kama wenzio wanakuzomea – Mungu amekusamehe, wala hazikumbuki dhambi zako tena.
Unaweza ukasema, lakini ndugu Mwakasege, hiyo mistari iko katika agano la kale, Je! tuna mistari kama hiyo katika Agano Jipya?
Hiyo mistari ipo mingi tu – lakini fahamu pia ya kuwa hiyo mistari ingawa iliandikwa wakati wa agano la kale ilikuwa inazungumza na watu walio katika agano jipya. Hii ni kwa sababu katika agano la Kale – pamoja na sadaka zilizokuwa zinatolewa, Mungu alikuwa anazikumbuka dhambi zao. Soma Waebrania sura ya 8,9, na ya 10.
Katika agano jipya, yaana wakati huu, mtu anapookoka, damu ya Yesu Kristo iliyo mbele ya kiti cha enzi kwa ajili yetu – inafuta hati zote zilizopelekwa na kuandikwa mbele za Mungu ambazo zilikuwa zimejaa dhambi zetu.
Ndiyo maana imeandikwa;
“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye; akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu, akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani” (Wakolosai 2:13,14).
Tafsiri ya Kiswahili cha kisasa inasema hivi katika mistari hii ya Wakolosai 2:13,14;
“Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi uzima pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kupigilia Msalabani.
Soma pia Waebrania 9:23 – hati iliyotumwa mbinguni na shetani kukushitaki imefutwa! Shetani anapojaribu kukukumbusha juu ya dhambi za zamani ulizozifanya kabla ya kuokoka, ujue ameshika nakala tu ya hati, lakini hati yenyewe ilikwishafutwa kwa damu ya Yesu.
Mbele ya Mungu unaonekana huna kosa, kwa sababu hujasimama mwenyewe mbele zake – lakini Yesu aliyekuokoa yuko pamoja na wewe – kwa kuwa uhai wetu, “umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu” (Wakolosai 3:3)
Hebu zidi kutiwa moyo na maneno yafuatayo yaliyomo katika Warumi 8:31-39 yanayosema: “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.
“Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo?…. lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
2. Juu ya Roho Mtakatifu aliye ndani yako.
Katika sura zilizotangulia za kitabu hiki nilikwambia ya kuwa kati ya mambo yaliyotokea wakati ulipookoka ni kwamba Roho Mtakatifu aliingia ndani yako – maana ndiye aliyekuzaa mara ya pili, umekuwa kiumbe kipya, na uzima wa milele umo ndani yako.
Biblia inasema hivi;
“Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye mihuri hii, Bwana awajua walio wake” (2Timotheo 2:19).
Kinachomfanya Mungu awajue walio wake ni kwa kuangalia muhuri aliouweka katika mioyo yao. Ndiyo maana itakuwa rahisi kutubagua siku ya kutubagua kama kondoo na mbuzi.
Mfugaji yoyote anajua ya kuwa akitaka mifugo yake iwe rahisi kuitambua hata kama itajichanganya na ya wengine ni kwamba lazima aipige muhuri usiofutika kirahisi mifugo yake. Kwa sababu ya muhuri huo – inakuwa rahisi kuijua mifugo iliyo yake.
Biblia inatuambia ya kuwa Yesu Kristo ni mchungaji mkuu wa kondoo wake, ambao ni sisi – na pia ametupiga mihuri mioyoni mwetu ili iwe rahisi kwetu kutambulikana kwake, na kwa shetani pia.
Imeandikwa hivi;
“Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, ‘Baba’ (Wagalatia 4:6)
Tena imeandikwa hivi;
“Nanyi pia katika huyo mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake kuwa sifa ya utukufu wake” (Waefeso 1:13,14).
Je! umejionea mwenyewe maneno haya?…. “mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa MUHURI na roho yule wa ahadi aliye mtakatifu.” Ikiwa umepigwa au umetiwa muhuri na Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu aliye ndani yako, ni nani atakayethubutu kusema hujaokoka sawasawa na ubabaike? Jibu ni hakuna!
Pia, fahamu ya kuwa si tu kwamba Roho Mtakatifu ametutia muhuri wa Mungu ambao kwa huo uzima wa milele uliomo ndani yetu anatutambua tu wake, - lakini pia Roho Mtakatifu “ndiye aliye ARABUNI ya urithi wetu….”
Neno “arabuni’ maana yake dhamana. Ngoja nikupe mfano utakaokusaidia kuelewa vizuri uzito na maana ya neno hili
Ikiwa una ndugu au rafiki aliyeshikwa na polisi na kuwekwa ndani, kufuatana na sheria ya nchi, unaweza kumwekea mdhamana mahakamani kwa kuweka ahadi ya kuwa wewe ndiye utakayefuatilia maisha yake akiwa nje kwa dhamana, na kwamba akitakiwa mahakamani atakuwepo, na asipokuwepo wewe ndiye utakayewajibika. Kumbuka na sisi kabla ya kuokoka tulikuwa tumefungwa katika minyororo ya dhambi – na Yesu Kristo alikufa na kufufuka ili kututoa katika minyororo hiyo – na ametutumia ahadi ya Roho mioyoni mwetu kututia MUHURI ili tusipotee bali tuwe na uzima wa milele na tabia mpya na mwenendo mpya ili ijulikane ya kuwa sisi ni wake pia, Roho Mtakatifu ndiye arabuni – mdhamini wa urithi wetu (- tuko nje ya mnyororo wa dhambi kwa sababu Yesu ametudhamini kwa Roho huyo aliyetupa) – “ ili kuleta ukombozi wa milki yake” siku ya hukumu ikifika tutakaposimama mbele ya mahakama ya mbinguni.
Sasa unaweza ukaelewa vizuri mistari ifuatayo:
“Basi yeye atufanyae imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu” (2 Wakorintho 1:21,22).
Tafsiri nyingine inasema hivi hasa mstari huu wa 22 ya kuwa “naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa uhakika wa udhamini wake kwa kutupa roho wake mioyoni mwetu”
Je! sasa unaelewa? Ukisoma pia 2 Wakorintho 5:5 utaona wazo hili likijitokeza tena; “Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya neno lilo hilo ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho”.
Suala la wewe kuwa na uhakika ya kuwa umeokoka si suala la kuona jinsi unavyojisikia bali ni suala la wewe kuamini neno la Mungu ya kuwa kimetokea moyoni mwako kile ambacho neno linasema kimetokea.
Suala la wewe kuwa na uhakika wa wokovu wako si suala la kupata maoni kutoka kwa wanadamu, bali ni suala la wewe kujua neno la Mungu (Biblia) linasema nini juu ya mtu aliyeokoka na kuliamini.
Kwa hiyo ikiwa umeifanya sala ya toba na kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama Bwana na Mwokozi wako, biblia inasema; 1. Umesamehewa dhambi zako zote na Mungu, na wala hazikumbuki tena; 2. Roho Mtakatifu yumo ndani yako na amekutia muhuri kuthibitisha ya kuwa wewe ni mtoto wake na amekudhamini maisha yako.
Ikiwa Yesu Kristo katudhamini kwa roho wake (Waefeso 1:13,14), tena ndiye wakili wetu anayetutetea (1Yohana 2:1,2) wa kutuombea (Waebrania 7:18) mbele za Baba Mungu …. na ikiwa Mungu Baba amekubaliana na upande wa utetezi (Warumi 8:31-34) – shetani aliye mshitaki wetu atatubabaisha nini?
Ndiyo maana imeandikwa hivi; “Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi … kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye, maana yu hai siku zote ili awaombee” (Waebrania 7:22,25)
Kwa hiyo usisumbuke kwa mawazo wala maneno yanayosema hujaokoka sawasawa – kwa sababu Bwana Yesu Kristo amekuokoa “KABISA”!
ATAKAYEVUMILIA MPAKA MWISHO
Kuna usemi unaosema ‘kuzaa ni rahisi kuliko kulea”. Wale wakina mama wenye watoto wanaelewa wazi ya kuwa kumlea mtoto ni kazi ngumu kuliko kumzaa.
Tukizungumza kwa jinsi ya rohoni tunaweza kusema kuokoka si kazi ngumu, bali kudumu katika wokovu ndipo penye mtihani mzito.
Katika maisha ya wokovu unaweza kukutana na vipingamizi vya kila namna ili mradi tu shetani apate namna ya kukukatisha tamaa uache wokovu. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema hivi;
“Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka” (Mathayo 24:13)
Yesu hakuwa anatuambia ya kuwa huwezi kuokoka mpaka ufikie mwisho wa maisha yako, au ufike mwisho wa dunia, bali alikuwa anatutahadharisha juu ya majaribu tunayoweza kukutana nayo katika maisha ya wokovu.
Ndiyo maana mistari mingi katika biblia imeandikwa kutukumbusha juu ya jambo hili. Kwa mfano hebu soma mistari ifuatayo:
“Naja upesi. Shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako” (Ufunuo 3:11).
Pia katika Kitabu cha Ufunuo 3:7,11,17, 26-28 na Ufunuo 3:5,12 na 21 utaona jinsi Yesu Kristo anavyoeleza na kututia moyo akieleza kitu gani kitatokea watu wake wakishinda mitego na mitihani ya maisha iliyoko mbele yao. Katika Ufunuo 2:10 anasema:
“Usiogope mambo yatakayokupata; tazama huyo ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiewe, … uwe mwaminifu hata kufa nitakupa taji ya uzima”.
Sikuandikii mambo haya kukuogopesha na kukutisha na pia nitakuwa sikuambii ukweli kama nitakuambia ya kuwa maisha ya wokovu ni mtelemko tu. Maisha ya wokovu si mtelemko wala lele mama – yana gharama yake. Lakini kilicho muhimu ni kujua ya kuwa unapookoka Yesu Kristo aliye ndani yako anakuwezesha kuishi maisha ya ushindi kila siku na kila mahali.
Nakushauri udumu katika mambo yafuatayo ili maisha yako ya wokovu yazidi kushamiri na kuimarika sasa na siku zote:
1. Dumu katika kusoma na kutafakari Neno la Mungu lililomo katika Biblia. Roho Mtakatifu uliye naye sasa atakusaidia na kukuhekimisha namna ya kuisoma Biblia – akikufunulia maana ya mistari hiyo unayoisoma.
2. Dumu katika maombi – kuzungumza na Mungu wako katika sala. Biblia ina mistari mingi sana inayoeleza faida ya kudumu katika maombi. Uwe mtu wa maombi, na utaona mabadiliko makubwa yakitokea hasa katika kuwa karibu zaidi ya uongozi wa Mungu na msaada wake.
3. Usiache kukutanika na watu wengine waliookoka katika kushirikiana neno la Mungu, kuonyana na kutiana moyo katika safari hii ya wokovu. Mungu atakuongoza katika jambo hili pia.
4. Kila mara unapoona nafasi ikitokea, kusudia kabisa, na tamani watu wengine waokoke kama vile wewe ulivyookoka. Kwa hiyo uwe tayari kuwashuhudia watu wengine habari za Bwana Yesu ili yamkini neema ya Mungu iliyo juu yao ikawasaidie wapate kutubu, na kumrudia Mungu wao na kuokoka.
Katika mambo yote hayo, ni maombi yangu kwa Mungu ya kuwa yeye mwenyewe atakutunza na kukusaidia ili maisha yako yawe ya ushuhuda, kila siku na kila mahali.
Kumbuka umekuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo na unaposema umeokoka – shetani anategemea tabia yako ibadilike na wanadamu waokuzunguka wanategemea tabia yako ibadilike. Isipobadilika wanaanza kuwa na wasiwasi na wokovu wako. Watafikiri unatania. Mimi naamini umeokoka kweli na wala hutanii – ndiyo maana umekisoma kitabu hiki bila kuchoka mpaka umefikia hapa – kwa hiyo maisha yako yabadilike na tabia zako zibadilike.
Neno la Mungu katika Yakobo 2:17,26 linasema; “ Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake …. Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa”.
Maana yake unatakiwa uwe mtendaji wa neno na usiwe msikiaji tu ukitaka maisha yako ya kiroho yajengwe juu ya msingi imara na usiotikisika.
MWISHO
TUNAKUTAKIA BARAKA NA USHINDI
Mimi na mke wangu, Diana, pamoja na watoto wetu Esta, Ana, Sara na Joshua tukishirikiana na wenzetu wa timu ya maombi tunaodumu nao katika kazi ya Mungu – tunapenda kukutia moyo na kukutakia baraka za Bwana na ushindi tele katika maisha haya mpya ya wokovu uliyoanza.
Jipe moyo mkuu kwa kuwa, Mungu amekusudia mambo mazuri juu yako. Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, uweze kumjibu kila mtu akuulizaye juu ya uhusiano wako na Mungu katika Kristo Yesu.
Na sisi hatutaacha kutoa shukrani zetu kwa Mungu kwa kukuokoa, tukikukumbuka katika sala ya kuwa Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, akupe wewe, roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya moyo wako yatiwe nuru ujue tumaini la mwito wa wokovu wake juu yako jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yako jinsi ulivyo; kwa kadri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa Roho.
Basi, Mungu huyu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa Kondoo kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, akufanye wewe kuwa mkamilifu katika kila tendo jema, upate kuyafanya mapenzi yake; naye Mungu akifanya ndani yako lipendezalo mbele zake; kwa Yesu Kristo; Utukufu una yeye milele na milele Amina.
Ikiwa utapenda kutushirikisha mahitaji yako ya maombi ili tushirikiane nawe katika maombi basi niandikie:
Christopher na Diana Mwakasege,
S.L.P. 2166,
ARUSHA.
©2003-2011 Tanzania Social and Economic Trust. All Rights Reserved.
Comments
Post a Comment